
Afisa mazingira Wilayani Kishapu Mkoani Shinyanga Charles Kanwakabo
Katika kuhakikisha mazingira yanabaki kuwa safi na salama kwa afya ya jamii, Wilaya ya Kishapu Mkoani Shinyanga imepiga hatua muhimu kwa kuanzisha mchakato wa ujenzi wa dampo la kisasa na la kudumu katika eneo la Sulagi, hatua inayolenga kuimarisha usimamizi wa taka na kulinda mazingira kwa vizazi vya sasa na vijavyo.
Afisa Mazingira wa Wilaya ya Kishapu, Charles Kanwakabo, amesema desturi ya kufanya usafi wa maeneo yote ya shughuli za kijamii imeendelea kuungwa mkono kwa kiwango cha kuridhisha.
Ametoa pongezi kwa wananchi, wanafunzi na viongozi waliojitokeza kushiriki zoezi la usafi lililofanyika Julai 26, 2025, akibainisha kuwa hali ya usafi imefikia kiwango cha asilimia 85 ishara ya mwamko mpya wa utunzaji wa mazingira miongoni mwa jamii.
“Tunashukuru wananchi, viongozi na wanafunzi wa Kishapu Sekondari kwa kushiriki kikamilifu. Licha ya mafanikio haya, tunasisitiza kuwa usafi usiwe tu wa kila mwisho wa mwezi bali uwe sehemu ya maisha ya kila siku,” amesema Kanwakabo.
Aidha, ametoa wito kwa wakazi wa Kishapu kuacha kusubiri maagizo ya viongozi ili kushiriki katika usafi, bali kujenga tabia endelevu ya kuhifadhi mazingira kwa maslahi ya pamoja.
Kwa upande wake, Mtendaji wa Mamlaka ya Mji Mdogo Kishapu, Godwin Everygist, amesema kuwa tayari mamlaka imeanza mchakato wa ujenzi wa dampo la kisasa katika eneo la Sulagi, hatua inayolenga kupunguza changamoto za utupaji holela wa taka na kukuza miji safi na salama.

Mtendaji wa Mamlaka ya Mji Mdogo Kishapu, Wilayani Kishapu Mkoani Shinyanga Godwin Everygist
“Katika kipindi hiki cha mpito, tunasisitiza uhifadhi sahihi wa taka kwenye dampo la muda, huku tukielekea kwenye mji wa kisasa wenye miundombinu bora ya usimamizi wa taka,” amesema Everygist.
Ameongeza kuwa ni muhimu kwa kila kaya kuhakikisha inakuwa na choo bora na salama ili kuzuia uharibifu wa mazingira na milipuko ya magonjwa yanayochochewa na uchafu.

Baadhi ya Wanafunzi kutoka Shule ya Sekondari Kishapu Wilayani Kishapu Mkoani Shinyanga wakifanya usafi
Zoezi la usafi wa pamoja lililofanyika Julai 26 limehusisha maeneo muhimu ikiwemo Soko la Swalala, uwanja wa Shirecu, pamoja na dampo la muda, ikiwa ni sehemu ya jitihada za kujenga utamaduni wa kudumu wa usafi na kujali afya ya jamii katika Wilaya ya Kishapu.

Halmashauri ya Wilaya Kishapu
Anwani ya Posta: S.L.P. 1288 KISHAPU
Simu ya mezani: +255282770020
Simu: +255282770020
Barua pepe: info@kishapudc.go.tz/ded.kishapudc@shinyanga.go.tz
Hakimiliki © 2016 Halmashauri ya wilaya ya Kishapu. Haki zote zimehifadhiwa