Mkuu wa mkoa wa Shinyanga Mhe. Mboni Mhita akizungumza kwenye ziara ya ukaguzi wa mradi wa ujenzi wa kituo cha afya Masagala kilichopo kata ya Maganzo wilaya ya Kishapu, leo Januari 10, 2026.
Mkuu wa mkoa wa Shinyanga Mhe. Mboni Mhita amefanya ziara ya ukaguzi wa miradi ya maendeleo wilaya ya Kishapu leo Januari 10, 2026 katika kituo cha afya Masagala kinachojengwa katika Kijiji cha Masagala kata ya Maganzo, ujenzi wa soko la wafanyabiashara Maganzo na ujenzi wa madarasa 3 na matundu 6 ya vyoo katika Kijiji cha Mwamasololo kilichopo kata ya Sekebugoro.
Akizungumza wakati wa kukagua ujenzi wa kituo hicho cha afya kinachojengwa kwa ufadhili wa kampuni ya Mwadui kupitia mpango wa uwajibikaji wa makampuni kwa jamii (CSR), Mhe. Mhita lengo la mradi huo ni kutatua changamoto kwa kuimarisha huduma za afya kwa wanakijiji. Amesema kuwa ameridhishwa na kasi ya ujenzi wa kituo hicho huku nakiwashukuru wananchi wa Masagala kwa kuanza awali kuibua mradi wa ujenzi huo.
“Nimeridhishwa sana kwa kasi na ubora wa ujenzi wa kituo hiki. hii ni jitihada kubwa. Ninatarajia mda mfupi ujao wananchi hawatotembea umbali mrefu kufuata huduma za afya”.Alisema Mhe. Mhita
Mkuu wa mkoa wa Shinyanga Mhe. Mboni Mhita akikagua ujenzi wa kituo cha afya Masagala kilichopo katika Kijiji cha Masagala kata ya Maganzo wilayani humo leo Januari 10,2026.
Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Kijiji cha Masagala Bw. Juma Kapima amesema kukamilika kwa kituo hicho kutapunguza adha ya wananchi waliokua wakifuata huduma hospitali ya Kolandoto na Mwadui.
Jumla ya sh. milioni 177,600,000 zinatarajiwa kutumika hadi kukamilika kwa kituo hiki cha afya Masagala ifikapo mwishoni mwa mwezi Februari, 2026, ambapo majengo yanayojengwa ni OPD, RCH, maabara, vyoo matundu 5 na kichomea taka.

Mkuu wa mkoa wa Shinyanga Mhe. Mhita akiwa katika picha ya pamoja na Mkuu wa Wilaya Mhe. Peter Masindi, wadau kutoka kampuni ya Mwadui pamoja na wananchi wa kijiji cha Masagala Januari 10, 2026.
Katika mradi wa ujenzi wa soko la kisasa la wafanyabiashara Maganzo kupitia mpango wa CSR Mhe. Mhita ameridhishwa na maendeleo ya ujenzi huo huku akitoa agizo kwa Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri kuhakikisha kuwa wafanyabiashara wa zamani wa soko hilo wanapewa kipaumbele cha kurejea katika soko hilo jipya pindi ujenzi utakapokamilika.
“Wafanyabiashara waliopisha ujenzi huu wapewe nafasi kwanza kwasababu ndio walikuwa kwenye soko hili awali, wakilipa ushuru na kuchangia mapato ya Halmashauri”.Alisema Mhe. Mhita
Akisoma taarifa ya utekelezaji wa mradi huo, Bi.Hilda Hozza kutoka mgodi wa Mwadui alisema soko hilo linajengwa kwa gharama ya sh. Milioni 260.Aliongeza kuwa hadi sasa ujenzi umefikia asilimia 70 na unatarajiwa kukamilika mwishoni mwa mwezi Februari,2026.

Mkuu wa mkoa wa Shinyanga Mhe.Mboni Mhita akizungumza kwenye ziara ya ukaguzi wa mradi wa ujenzi wa soko la wafanyabiashara la Maganzo lililopo kata ya Maganzo wilaya ya Kishapu leo Januari 10, 2026

Mkuu wa mkoa wa Shinyanga Mhe. Mboni Mhita akinunua bidhaa kwa mmoja wa wafanyabiasha waliopisha ujenzi wa soko jipya la kisasa katika eneo la Maganzo, leo Januari 10,2026.

Muonekano wa soko la kisasa la wafanyabiashara linalojengwa katika eneo la Maganzo, kata ya Maganzo, wilaya ya Kishapu.
Katika hatua nyingine, Mkuu huyo wa mkoa amepata fursa ya kusikiliza kero za wanchi kwenye mkutano wa hadhara uliofanyika katika Kijiji cha Mipa kata ya Sekebugoro, ambapo wanakijiji waliwasilisha kero na changamoto zao hususani upande wa barabara, maji yaani ukosefu wa maji kutoka ziwa victoria kwenye baadhi ya vijiji, elimu yaani upungufu wa walimu, vituo vya afya yaani upungufu wa madaktari, pamoja na ombi la uimarishwaji wa ulinzi katika makazi yao.
Aidha Mhe. Mhita amezitaka mamlaka husika za taasisi zilizopo ndani ya Wilaya ya Kishapu kushughulikia mahitaji hayo ya wananchi, huku akisema kazi yake ni kurejesha imani na tabasamu kwa wananchi.
Halmashauri ya Wilaya Kishapu
Anwani ya Posta: S.L.P. 1288 KISHAPU
Simu ya mezani: +255282770020
Simu: +255282770020
Barua pepe: info@kishapudc.go.tz/ded.kishapudc@shinyanga.go.tz
Hakimiliki © 2016 Halmashauri ya wilaya ya Kishapu. Haki zote zimehifadhiwa