Halmashauri ya Wilaya ya Kishapu imepokea shehena ya chanjo za mifugo kutoka Serikalini kupitia Wizara ya Mifugo na Uvuvi, ikiwa ni sehemu ya kampeni ya kitaifa ya kudhibiti magonjwa ya mifugo. Kampeni hii ya miaka mitano inalenga kuimarisha afya ya mifugo na kuinua kipato cha wafugaji.

Chanjo zilizopokelewa ni pamoja na dozi 450,000 za chanjo dhidi ya homa ya mapafu ya ng’ombe (CBPP), dozi 442,000 za chanjo dhidi ya ugonjwa wa Sotoka kwa mbuzi na kondoo (PPR), pamoja na dozi 300,000 za chanjo ya kuku aina ya “Tatu Moja” inayokinga dhidi ya magonjwa ya mdondo, ndui na mafua ya kuku.

Katika kuhakikisha wafugaji wengi zaidi wanapata huduma hiyo muhimu, Serikali imetoa ruzuku kwa chanjo hizo. Dozi ya chanjo kwa ng’ombe itatolewa kwa shilingi 500 badala ya shilingi 1,000. Chanjo kwa mbuzi na kondoo itatolewa kwa shilingi 300 badala ya 600, huku chanjo ya kuku ikitolewa bure kabisa.

Wananchi wa Wilaya ya Kishapu wanahimizwa kujitokeza kwa wingi kuwapatia mifugo yao chanjo hizo ili kujikinga dhidi ya milipuko ya magonjwa na kuongeza uzalishaji wa mifugo.

Hatua hii ni sehemu ya juhudi endelevu za Serikali katika kuimarisha sekta ya mifugo, ambayo ni chanzo muhimu cha kipato kwa wananchi na mchango mkubwa katika ukuaji wa uchumi wa taifa.
Halmashauri ya Wilaya Kishapu
Anwani ya Posta: S.L.P. 1288 KISHAPU
Simu ya mezani: +255282770020
Simu: +255282770020
Barua pepe: info@kishapudc.go.tz/ded.kishapudc@shinyanga.go.tz
Hakimiliki © 2016 Halmashauri ya wilaya ya Kishapu. Haki zote zimehifadhiwa