Mkuu wa TAKUKURU Wilaya ya Kishapu Mkoani Shinyanga Atuganile Stephen akizunguza kwenye semina iliyohusisha Viongozi wa dini,Viongozi wa siasa na Waandishi wa Habari kuhusiana na makosa ya Rushwa kuelekea Uchaguzi Mkuu walipokuwa ofisi za Taasisi hiyo Oktoba 2,2025
Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU) Wilayani Kishapu Mkoani Shinyanga imeendesha semina maalum kwa viongozi wa dini, viongozi wa vyama vya siasa na waandishi wa habari ikiwa ni sehemu ya maandalizi kuelekea Uchaguzi Mkuu utakaofanyika Oktoba 29, 2025.
Akizungumza katika kikao hicho kilichofanyika Ofisini hapo Oktoba 2,2025, Mkuu wa TAKUKURU Wilaya ya Kishapu, Atuganile Stephen, amesema lengo la semina hiyo ni kutoa elimu ya kina kuhusu makosa ya Rushwa yanayoweza kujitokeza katika kipindi cha uchaguzi na athari zake kwa jamii.
Atuganile amebainisha kuwa Rushwa wakati wa uchaguzi siyo tu kosa la kisheria bali pia ni udhalilishaji wa haki ya msingi ya wananchi kuchagua viongozi wao kwa uhuru.
"Kila mdau ana jukumu la kuhakikisha uchaguzi unakuwa huru na wa haki bila kushawishiwa kwa Rushwa ya aina yoyote, huku akiwataka viongozi wa dini kutumia nafasi zao kuelimisha waumini kuhusu madhara ya kupokea au kutoa Rushwa huku akiwataka viongozi wa vyama vya siasa kuendesha kampeni zenye kuzingatia maadili na sheria badala ya kutumia mbinu za kifisadi kuwanunua wapiga kura.
Kwa upande wake, Afisa wa TAKUKURU Wilayani Kishapu Neema Samamba, akiwasilisha mada kuhusu makosa ya Rushwa, ameeleza kwa kina baadhi ya vitendo vinavyokatazwa kisheria ikiwemo kutumia wadhifa kushawishi uteuzi wa wagombea, mwenendo usiofaa wa Maafisa waandikishaji, makosa yanayohusu daftari na kadi za wapiga kura pamoja na ukiukaji wa taratibu za usimamizi wa uchaguzi.

Afisa wa TAKUKURU Wilayani Kishapu Neema Samamba akizunguza kwenye semina iliyohusisha Viongozi wa dini,Viongozi wa siasa na Waandishi wa Habari kuhusiana na makosa ya Rushwa kuelekea Uchaguzi Mkuu walipokuwa ofisi za Taasisi hiyo Oktoba 2,2025
“Lengo la kuwaelezea haya yote ni kutokana na umuhimu wenu kwa jamii na jinsi mnavyoaminika na watu mnaowaongoza, ili muwe mabalozi wa kutoa elimu hii kwa wananchi. Ni wajibu wenu kuhakikisha kila mmoja anafahamu makosa ya Rushwa pamoja na adhabu zilizowekwa chini ya Sheria ya Uchaguzi wa Rais, Wabunge na Madiwani Namba 1 ya mwaka 2024,” amesisitiza Samamba.
Semina hiyo imepokelewa kwa hamasa kubwa na washiriki ambapo viongozi wa dini wameahidi kuwa mabalozi wa maadili mema kwa waumini wao, viongozi wa vyama vya siasa wakiahidi kuzingatia sheria na maadili wakati wa kampeni, huku waandishi wa habari wakiahidi kuendelea kuelimisha wananchi kupitia uandishi unaozingatia ukweli na uwajibikaji.

Katika kuhitimisha kikao hicho, washiriki wamekubaliana kwa pamoja kuwa mapambano dhidi ya Rushwa ni jukumu la kila mmoja, na kwamba mafunzo hayo yatawasaidia kuhakikisha Uchaguzi Mkuu wa Oktoba 29, 2025 unafanyika kwa haki, uwazi na amani.
Halmashauri ya Wilaya Kishapu
Anwani ya Posta: S.L.P. 1288 KISHAPU
Simu ya mezani: +255282770020
Simu: +255282770020
Barua pepe: info@kishapudc.go.tz/ded.kishapudc@shinyanga.go.tz
Hakimiliki © 2016 Halmashauri ya wilaya ya Kishapu. Haki zote zimehifadhiwa